Jul 10, 2014

SIMBA SC YAMNASA CASILLAS NA KUMSAINISHA MIAKA MIWILI

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba wamekamilisha usajili wa kipa namba moja wa Mtibwa Sugar, Hussein Sharrif `Iker Casillas` na kumsainisha mkataba wa miaka miwili.
Kwa muda mrefu Simba ilionesha nia ya kumsajili mlinda mlango huyo bora wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu uliopita, lakini ilimkosa mara kadhaa na sasa ndoto zimetimia.
Casillas aliyekuwa tegemeo katika klabu ya  Mtibwa Sugar ameungana na makipa Ivo Mapunda na Abuu Hashim katika kikosi cha Simba.
Simba ilimtema kipa wake, Mghana, Yaw Berko baada ya kumalizika kwa msimu wa 2013/2014 wa ligi kuu Tanzania bara, hivyo kubakiwa na makipa wawili tu.
Kusajiliwa kwa Casillas ambaye aliwahi kuitwa katika kikosi cha Taifa stars chini ya Kim Poulsen kutaleta upinzani mkubwa baina yake na kipa namba moja wa Simba, Ivo Mapunda.
Uwezo mkubwa aliouonesha kwa wakati wote akiidakia Mtibwa Sugar, Casillas anatarajiwa kuisaidia Simba inayohitaji mafanikio msimu ujao.
Wakati huo huo, Simba imemsainisha kipa kinda, Peter Manyika Junior ili ajiunge na Simba B.