Jul 9, 2014

Mwenyekiti TLP ampa mbuzi Magufuli

MWENYEKITI Chama cha Tanzania Labour (TLP) wa Mkoa wa Mara, Mafwili Munyaga, amekabidhi mbuzi wawili Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na kumuomba agombee nafasi ya juu katika uchaguzi mkuu ujao.

Kiongozi huyo wa chama cha upinzani, alimpongeza Magufuli na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola kwa uchapakazi.

Munyaga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mwibara kupitia TLP, alisema hayo juzi wakati akimkabidhi waziri huyo mbuzi wawili baada ya kumaliza kuhutubia wananchi katika Mji mdogo wa Kibara.(Martha Magessa)

Akiwa amevalia fulana yenye maandishi mbele ‘Magufuli Karibu Mwibara’ na nyuma ‘Magufuli Jembe la Watanzania’, Mwenyekiti huyo wa TLP alisema Magufuli na Lugola, ni wachapakazi wanaotekeleza kauli mbiu ya Tanzania wataifanyia nini na siyo itawafanyia nini wao.

Alisema kutokana na uchapakazi mzuri, Magufuli anafaa kugombea nafasi ya juu zaidi serikalini, ambayo hakutaja ni ipi.

Hata hivyo, akizungumza na mwandishi, Munyaga alisema kulingana na tabia na uwezo alionao waziri huyo, anapaswa agombee nafasi ya urais, katika uchaguzi mkuu ujao.

“Yaani kwa ujumla wake, yeye ndiye anayefaa kabisa kuwa Rais wetu,” alisema. Munyaga alishukuru uamuzi wa kuwapatia boti, inayounganisha Jimbo la Mwibara na Musoma Vijijini. Kuhusu Lugola, Mwenyekiti huyo wa TLP alisema pia anastahili kuendelea kuongoza jimbo hilo.

Alisisitiza kwamba, pamoja na kwamba yeye ni Mwenyekiti wa TLP Mkoa wa Mara, lakini lazima asifie Serikali ya CCM, kwani nchi inatekeleza Ilani ya chama hicho tawala. Awali, akihutubia wananchi, Magufuli pia alimsifia Lugola akisema ni mchapakazi shujaa katika kutetea hoja .

Alihoji kama Mwibara hawamtaki ili ampeleke kwenye jimbo lake la Chato.

“Ndugu zangu niwaambie kwa ujumla mnaye mbunge mzuri kabisa, pamoja na kwamba nabii hasifiwi kwao, huyu mbunge anafanya kazi nzuri sana…na kama ninyi hammtaki, mimi nitamuita kwenye jimbo langu,” alisema.

Magufuli alikuwa katika Jimbo la Mwibara kwa ziara ya siku moja, ambako alizindua kivuko cha Mv Mara, kitakachofanya kazi kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Musoma Vijijini. Katika uzinduzi wa kivuko kipya cha Mv Mara, Waziri Magufuli aliwataka wakazi wa Iramba na Majita, kukitunza kiwasaidie kuinua uchumi katika maeneo hayo.

“Ndugu zangu wa Iramba, kitunzeni kivuko hiki kwani ni mkombozi mkubwa katika kuwaletea maendeleo yenu pamoja na maeneo ya jirani,” alisema Waziri Magufuli.

Magufuli alisema kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba tani 25, yaani magari manne na abiria 50, kitaokoa maisha ya wananchi wengi ambao walikuwa wanapata adha kubwa ya usafiri kutokana na kukosa usafiri wa uhakika.

“Nimeambiwa hapa nauli ilikuwa Shilingi 2000 kuvuka upande wa pili kwa kutumia boti za watu binafsi lakini kwa kivuko hiki natangaza rasmi kuwa nauli kwa kivuko chetu kipya ni Shilingi 500 tu, na wanafunzi waliovaa sare watapanda bure na watoto shilingi 100,” alisema.

Waziri alisema nauli za magari na mizigo zitapangwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ambao ni wasimamizi wa kivuko hicho.

Chanzo:Habarileo