Balozi Ombeni Sefue
Gavana wa
zamani wa Benki Kuu ya Tanzania BOT), Marehemu Daudi Ballali aliacha
wasia unaotaka maiti yake isionyeshwe hadharani atakapofariki dunia na
wala maiti yake isiletwe Tanzania kwa ajili ya maziko.
Ballali
aliyefariki Mei 16, 2008 na kuzikwa Mei 23
mwaka huohuo katika makaburi
ya Gate of Heaven, eneo la Silver Spring, Maryland nchini Marekani
alifahamu kuhusu kifo chake wiki mbili kabla, baada ya matibabu
kushindikana.
Mwandishi
wa Mwananchi aliyekuwa nchini Marekani kwa siku kumi kufuatilia suala
hilo, alibaini kuwa kiongozi huyo alilazwa mara ya pili katika Hospitali
ya Chuo Kikuu cha George Washington, April 2008 na alirejea nyumbani
kwake, Washington DC wiki mbili kabla ya kukutwa na mauti.(P.T)
Habari
kutoka ndani ya familia yake zinasema baada ya madaktari kushindwa
kumtibu walimwambia kwamba asingeweza kuishi kwa zaidi ya wiki mbili,
hivyo walimshauri ahamie kwenye 'hospice' ambayo ni nyumba maalumu ya
kusubiri kifo kwa watu ambao magonjwa yao yameshindikana.
Hospice
hutumika kwa ajili ya kuwaweka wagonjwa wanaohitaji faraja hasa kutoka
na maumivu makali chini ya uangalizi wa washauri na wauguzi kwa lengo la
kuwaongezea wagonjwa husika siku za kuishi.
Baadhi ya
hospice hutoa huduma za kiroho, kijamii na kifedha na wakati mwingine
huduma hizo hutolewa kwa wagonjwa ambao wanaugulia nyumbani. Hata hivyo,
gazeti hili lilidokezwa kwamba Ballali alikataa kwenda kwenye nyumba
hiyo na badala yake kutaka apelekwe nyumbani kwake.
"Alikataa
kwenda kwenye hospice, aliwaambia madaktari kwamba yeye hawezi kwenda
huko ijapokuwa kuna huduma nzuri na uangalizi wa nesi (muuguzi).
Aliwaambia kwamba nitakwenda kufia nyumbani kwangu maana nina nyumbani
kwangu," kilisema chanzo chetu na kuongeza:
"Aliporejeshwa
nyumbani, alikuwa anazungumza kama kawaida lakini kadri siku
zilivyosogea hali ilikuwa ikibadilika na kama sikosei siku mbili au tatu
za mwisho (za uhai wake) alikuwa anajitambua lakini alikata kauli,
hakuwa akizungumza chochote".
Uchunguzi
wetu umebaini kuwa katika siku hizo za mwisho za uhai wake, Ballali
aliacha maelekezo kwamba pindi atakapofariki dunia, mwili wake usiwekwe
hadharani kwa maana ya kutazamwa na watu nje ya familia wala
kusafirishwa kuja Tanzania kwa ajili ya maziko.
"He said,
he doesn't like to be turned into a laughing staff (alisema asingependa
kugeuzwa kichekesho), sababu watu wasingekuja kutoa heshima za mwisho,
bali wangekuja kumdhihaki kuangalia Ballali aliyetuhumiwa kwa ufisadi wa
EPA na siyo Gavana," kilisema chanzo hicho.
Kifo, mazishi yake
Habari
kutoka ndani ya familia yake zinasema Ballali alifariki Mei 16, 2008 saa
8:00 mchana saa za Marekani, sawa na saa 03:00 za Tanzania akiwa
nyumbani kwake, Maryland.
Baada ya
kifo chake, mwili wake ulihifadhiwa kwenye nyumba ya maiti iitwayo Vol
Funeral Home iliyopo Washington DC kwa siku nne na siku ya tano Mei 23
uliondolewa na kupelekwa Kanisani kwa ajili ya Ibada kisha kupelekwa
makaburini kwa ajili ya maziko.
Siku hiyo
ya Mei 23 saa nne asubuhi, familia ya Ballali ikiongozwa na mjane wake
Anna Muganda pamoja na watoto wake wawili, mtalaka wake na wanafamilia
wengine, walikwenda Vol Funeral Home ambako walitoa heshima za mwisho
kwa marehemu.
"Katika
tukio hilo familia ilikubaliana kwamba matakwa ya marehemu yaheshimiwe,
kwa hiyo hakuna aliyeruhusiwa kupiga picha zozote. Kwa hiyo ni ndugu tu
wa familia walioruhusiwa kuona mwili wa Ballali, baadaye tulifunga
casket (jeneza) na tukaondoka kwenda Kanisani,"kilisema chanzo chetu
nchini Marekani.
Kauli
hiyo inaungwa mkono na maelezo yaliyotolewa kwa gazeti hili Agosti 25,
2013 na dada wa Marehemu Ballali, Margaret Mpango kwamba shughuli za
kuaga mwili wa marehemu, ibada na baadaye maziko vilikuwa ni kwa ajili
ya familia pekee.
Akizungumza
na Mwandishi wa Mwananchi, nyumbani kwake mjini Kigoma, Margaret Mpango
aliweka bayana kwamba: "Familia isingeweza kuruhusu watu wengine
kushiriki, haikuwa na maana yoyote kwani tayari kulikuwa na maneno mengi
yanayomhusu".
Dada huyo
anayezaliwa tumbo moja na Marehemu Ballali ni mke wa Askofu Mstaafu wa
Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kasulu, Kigoma, Dk. Gerald
Mpango ambaye alikuwa miongoni mwa walioongoza Ibada ya maziko ya
Ballali.
Margaret
alilithibitishia gazeti hili kwamba mumewe (Dk. Mpango), alishirikiana
na mapadre wa Kanisa la Mtakatifu Stephen, Washington D.C. kuongoza
ibada ya mwisho ya Ballali ambaye siku hiyohiyo alizikwa katika makaburi
yanayomilikiwa na Kanisa Katoliki ya Gate of Heaven.
Alisema
miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo ni aliyekuwa Balozi wa Tanzania
nchini Marekani wakati huo, Balozi Ombeni Sefue, ambaye hivi sasa ni
Katibu Mkuu Kiongozi.
Kauli ya Sefue
Jana
Balozi Sefue akizungumza na Mwandishi wa Mwananchi, alithibitisha kwamba
kweli alishiriki kwenye Ibada ya kumuaga Ballali na baadaye kwenye
maziko ya Gavana huyo katika makaburi ya Gate of Heaven.
"Ni kweli
nilishiriki kwenye maziko kwa sababu mimi kama Balozi wa Tanzania
wakati huo ndiye nilikuwa mwakilishi wa Serikali pale Washington, lakini
jambo la pili ni kwamba binafsi nilimfahamu Ballali kwa muda mrefu, kwa
hiyo hata kama nisingekuwa balozi lazima ningekwenda kuzika tu,"
alisema Balozi huyo.
Picha zake zasakwa
Taarifa
zaidi ambazo gazeti hili lilizipata Washington DC, zinasema kulikuwa na
jitihada za kutaka kupiga picha mwili wa marehemu wakati wa kutoa
heshima za mwisho, lakini zilikwama baada ya ndugu wa marehemu kuzima
jaribio hilo.
"Mmoja wa
waliokuwapo kwenye msiba baada sisi kumaliza kutoa heshima za mwisho
alitaka kupiga picha kwa madai kwamba anataka kubaki na sura ya ndugu
yetu, lakini tulikataa na kumwambia kwamba tulishakubaliana kutofanya
hivyo kwa heshima ya marehemu," kilieleza chanzo chetu na kuongeza:
"Baadaye
tulipata taarifa kwamba wapo watu tena kutoka Tanzania ambao walikuwa
wakihitaji picha hiyo kwa udi na uvumba na walikuwa wameahidi kuinunua
kwa Dola za Marekani 35,000". Kiasi hicho ni sawa na Sh57.7 milioni kwa
viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni wastani wa Sh1650 kwa
dola moja.
Safari ya Marekani
Safari ya
Mwandishi wa Mwananchi nchini Marekani ilianza Alhamisi Juni 26, 2014
hadi Jumapili, Julai 6. Mwandishi wa habari hizi aliligundua kaburi hilo
baada ya kwenda makaburi ya Gate of Heaven kwa siku tatu mfululizo.
Siku ya
kwanza, mwenyeji wa mwandishi ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa
alimfikisha katika makaburi hayo, lakini kaburi la Ballali halikuonekana
na hata mwandishi alipokwenda siku ya pili peke yake, kaburi hilo pia
halikuonekana kwa kutokana na ukubwa wa eneo hilo.
Siku ya
tatu, Mwandishi wa Mwananchi alilazimika kuomba msaada wa Ofisi ya
Makaburi ya Gate of Heaven, ambayo ilimsaidia kuonyesha eneo lilipo
kaburi hilo, hivyo kuwezesha kupata picha zake.
Kaburi
lake liko katika msitari wa mwisho kabisa na Ukanda wa Kijani wa miti
iliyozunguka makaburi ya Gate of Heaven, likiwa limeandikwa jina la
kiongozi huyo, pamoja na maneno ya Kiingereza yanayosomeka "When the
heart weep for what it has lost, the soul rejoices for what it has
found"
Maana ya
maneno hayo ni kwamba, "Wakati moyo ukiomboleza kwa kile kilichopotea,
roho hufurahi kwa kile kilichopatikana". Kaburi hili limezungukwa na
makaburi mengine kadhaa ambayo si ya Watanzania, kwani kwa haraka
kutokana na mazingira yalivyokuwa, Mwandishi wa Mwananchi hakuweza kuona
kaburi jingine lenye majina yenye asili au kuwa na mwelekeo wa asili ya
Tanzania.
Fuatilia mfululizo wa habari hii itakapoendelea kesho.
Chanzo:Mwananchi
