Dec 2, 2013

YAFAHAMU MAISHA YA NGULI WA MUZIKI WA RHUMBA TABU LEY ROCHEREAU, TANGU KUZALIWA KWAKE HADI KIFO CHAKE!!..INGIA HAPA!!

 Tabu Ley Rochereau, alizaliwa Novemba 13 mwaka 1940 huko Bandundu katika Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo. Alianza maisha akiitwa Pascal Tabu. Tabu Ley alianza maisha yake ya muziki mapema sana na 1954 akiwa na umri wa miaka 14 tu aliandika wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha,  ambao akaurekodi na kundi maarufu la African Jazz lililokuwa chini ya Joseph ‘Grande Kalle’ Kasebele, (asichanganywe na Pepe Kalle). Aliendelea na shule na hatimae alipomaliza High School 1959, ndipo alipojiunga rasmi na African Jazz. Alikuwa mmoja awapo wa walioimba ule wimbo utunzi wa Grande Kalle, na uliotikisa anga la Afrika miaka ya 60, Independence Cha Cha. Uliogeuka na kuwa wimbo rasmi wa kusherehekea uhuru wa kongo.



 Baada ya kiasi kama miaka minne alijiengua bendi hii na akiwa na mpiga gitaa mahiri Nicholaus Kassanda aka Dr Nico, wakaanzisha African Fiesta, ambapo alikuweko hadi 1965, wakati Kongo imewaka moto kimuziki na ushindani kuwa mkali sana, akaachana na Dr Nico na kuanzisha African Fiesta National au mara nyingine ikiitwa Africa Fiesta Flash, na kutoa kile kibao maarufu Afrika Mokili Mobimba, ambacho kilivuka mauzo ya nakala milioni moja miaka ya sabini, na kuiingiza bendi hii kuwa kati ya bendi zilizopata mafanikio ya juu katika Afrika kwa wakati huo. Wanamuziki kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni kati ya wakongwe waliowahi kupitia katika kundi hili tishio.
 Kufikia mwaka wa 70, Tabu Ley alianzisha Orchestre Afrisa International wakati huo Afrisa na TPOK Jazz ndizo zilikuwa bendi maarufu zaidi Afrika. Afrisa waliteremsha vibao kama Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon, na Mose Konzo na  Tabu Ley

 Aliweza hata kupata tuzo toka serikali za nchi kama Chad iliyompa heshima ya Officer of The National Order, wakati Senegal ilimpa heshima ya Knight of Senegal, na akawa sasa anaitwa Siegneur Rochereau. Katikati ya miaka ya 80 Tabu Ley aligundua kipaji cha mwanamama aliyekuja kutikisa anga za Afrika naye si mwingine ila Mbilia Bel, baadae Tabu alimuoa Mbilia a wakapata mtoto mmoja. Nyimbo kama Nadina, Nakei Nairobi zinaonyesha kipaji gani alikuwa nacho binti huyu aliyekuwa mzuri kwa sura, aliyejua pia kucheza na kutawala jukwaa vizuri.

 1988 Tabu akamgundua muimbaji wa kike mwingine Faya Tess. Hapo Mbilia akaacha bendi na kuendelea na maisha yake ya muziki peke yake. Kipindi hiki, mtindo wa Soukus uliokuwa na mapigo yenye mwendokasi zaidi ya lile rumba la Afrisa na TPOK Jazz ulianza kuzishika nyoyo za vijana, bendi hizi kubwa zikaanza kufifia.
Mwanzoni mwa miaka ya 90 Tabu Ley alihamia Marekani akaishi Kusini mwa California, akabadili muziki wake katika kujaribu kujikita zaidi katika soko la ‘Kimataifa’, akatunga nyimbo kama Muzina, Exil Ley, Babeti Soukous.

1996 Tabu Ley alishiriki katika album ya kundi la Africando na kushiriki katika wimbo Paquita wimbo aliyokuwa ameurekodi miaka ya 60 akiwa na African Fiesta. Tabu alipata cheo cha Uwaziri katika utawala wa Laurent Kabila baada ya kuondolewa kwa Mobutu. Hata baada ya kifo cha Laurent Kabila November  2005 Tabu alipewa cheo cha Vice-Governor in charge of political, administrative, and socio-cultural questions, kwenye jiji la Kinshasa. Mwaka 2006  Tabu Ley  akashirikiana na rafiki yake wa  muda mrefu Maika munah na kutoa album yake ya mwisho iliyoitwa Tempelo, katika album hiyo binti yake Melodie aliimba nyimbo kadhaa katika album hiyo.


Tabu Ley hali yake ki-afya alianza kusumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi tangu mwaka 2008 ambapo ilipelekea kupelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo mwenyezi mungu kampenda zaidi, ambapo jumamosi ya tarehe 30 Novemba 2013 aliweza kufariki dunia kufuatia ugonjwa huo wa kiharusi.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.
Tafsiri kwa hisani ya Kitime.