Oct 16, 2013

Haya ni majina 6 ya watanzania waliohukumiwa adhabu ya KUNYONGWA hadi kufa na mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Tabora

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Simon
Lukelelwa *



MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imewahukumu adhabu ya kunyongwa
hadi kufa washitakiwa sita, baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa
kukusudia. Imetoa adhabu hiyo katika kikao chake kinachoendelea mkoani
Shinyanga.

Adhabu hiyo ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda
ya Tabora, Simon Lukelelwa katika kesi nne tofauti. Kesi hizo ni za
mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake vikongwe, kutokana na imani potofu
za kishirikina.

Mauaji hayo yalifanyika kati ya mwaka 2005 na 2007 katika Wilaya za
Bukombe, Shinyanga na Kahama, ambako wanawake wanne waliuawa kikatili
kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili.

Waliopewa adhabu hiyo ni Venance Nuba na Tegemeo Paulo, ambao walitiwa
hatiani kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Sophia Gundu Januari 25,2006
katika Kijiji cha Kazibizyo Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita.

Wengine wawili waliokumbwa na adhabu ya kifo cha kunyongwa ni Joseph
Lushika na Maziku Mpiga Chai baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa
kukusudia Monica Bulemela Mei 5, 2005 katika Kijiji cha Lutembela Wilaya
ya Bukombe.

Mshitakiwa mwingine aliyekumbwa na adhabu ya kunyongwa ni Mhande
Manyanya baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa kukusudia Wande
Bulugu Julai Mosi, 2007 katika Kijiji cha Ihapa Wilaya ya Shinyanga
mkoani hapa.

Mshitakiwa wa sita aliyekumbwa na adhabu ya kunyongwa baada ya
kupatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia ni Tembo Hussein, aliyetiwa
hatiani kumuua kwa kukusudia Anjelina Hungwi katika kijiji cha Itega
Wilaya ya Kahama